UCHAGUZI MKUU BAKWATA , MRUMA ATEMA CHECHE
...
🔅“Tukibaini mgombea anayefaa na anayetakiwa na waislamu amekatwa tunafuta uchaguzi”
🔅Asema: wagombea wajiandae kuwa “Watumishi” wa watu na siyo “Wafalme”
🔅Awataka viongozi kupitisha wagombea wanaofaa na siyo wagomea waliowaandaa kwa maslahi binafsi ili kujijengea kinga na kudumisha “Ufalme wao”
🔅Aonya kuchagua kwa misingi ya ukabila, majimbo na ujamaa
🔅 Asema BAKWATA ni moja anayefaa anaweza kuchaguliwa popote
🔅viongozi wa kuteuliwa“chekeche litafanya kazi”
Na : Harith Nkusa
Mwandishi maalumu wa Mufti
🔸HABARI KAMILI
Kufuatia kutolewa kwa waraka maalum unaelekeza kufanyika uchaguzi mkuu wa BAKWATA kuanzia mwezi ujao katibu mkuu wa BAKWATA Alhaj Nuhu Jabir Mrumaamefunguka na kusema bayana kwamba hataruhusu mchezo mchafu kwenye uchaguzi huo
Katibu mkuu amemwambia mwandishi maalum wa mufti kwamba wenye nafasi kwenye uchaguzi huu ni wagombea wanaoweza kwenda na kasi ya samaha mufti Zubeir mwenye dhamira na lengo la kujenga "BAKWATA mpya" na wakati wote watazingatia haja kubwa ya maendeleo iliyoko sasa.
Kwa mujibu wa waraka huo uliotolewa na katibu huyoTarehe 8/1/2020 na kuelekezwa kwa makatibu wa mikoa na wilaya zote nchini, uchaguzi kwenye ngazi ya misikti na kata utafanyika kuanzia tarehe 15/2/2020 mpaka 28/2/2020 wakati uchaguzi ngazi ya mikoa na wilaya utafanyika kati ya tarehe 15 mpaka 31/3/31/2020 na uchaguzi ngazi ya taifa utafanyika kati ya tarehe 14 na 30/4/2020. Kwa mujibu wa waraka huo chaguazi hizo za ngazi zote zitahusisha kuchaguliwa viongozi wa Jumuia za Vijana na wanawake.
Alha Mruma ameonya vikali kupitisha majina ya wagombea au kuwachagua kwa misingi ya ukabila, mkoa na ujamaa. Akasema viongozi wanaohusika kupitisha majina ya wagombea wachuje majina kwa kuzingatia sifa kwa mujibu wa katiba ikiwa ni pamoja na uchamungu, kujituma, kujitolea, ubunifu na uaminifu.
Amesema viongozi wasipitishe majina ya watu wao waliowandaa kwa maslahi yao binafsi ili waendelee kuwa mabwana wakubwa na wafalme wasioshaurika na wasiokosolewa kwenye maeneo yao
“Najua kuna viongozi tayari wana majina yao mifukoni. Lakini sisi tunasema Hata kama ni mpinzani wako maadamu ana sifa apitishwe kama mgombea. Acheni waislamu waamue. Acheni kusema huyu ni wangu na huyu si wa kwangu. Akiwa mdadisi na mwenye kuhoji anafaa. Lazima tukubali changamoto. Vinginevyo maendeleo yataendelea kuwa ndotoni”
Amesema na kuendelea “Uchaguzi uwe huru, kila mwenye sifa awe huru kugombea, jambo muhimu wagomea hao wajue majukumu na mipaka yao kikatiba. Tukibaini mahala palipo na aina yoyote ya upendeleo tunavunja uchaguzi na hatua kali zitafuata kwa kiongozi aliyehusika”
Akisisitiza onyo hilo alhaj Mruma alionyesha kukerwa na watu ambao bado wanafikiria na kuweka mbele maslahi yao binafsi
"Uchaguzi unalenga kuwapatia waislamu wa Tanzania viongozi sahihi. Viongozi watakaoleta maendeleo kwenye Uchumi, elimu, afya na huduma nyingine za kiibada na kijamii. Waislamu wanataka mengi ambayo yamekuwa yanakwama na watu wenye dhamira na uwezo wa kuwakwamua wapo. Kwa nini wasipewe nafasi? Ameuliza kwa masikitiko makubwa.
Amesema uhuru anaoutaja hatarajii utakuwa mlango wa kuwapenyeza mamluki na watu wasioitakia mema BAKWATA, waislamu na Tanzania kwa ujumla.
" Wagombea wawe na nia na dhamira ya kweli na ya wazi kutetea na kulinda BAKWATA, maslahi ya waislamu, amani na maendeleo endelevu ya taifa letu. Asichaguliwe mtu atakayetuvuruga. Umoja tunaoutaja usiwe mlango wa kuwaingiza watu wenye mawazo na fikra potofu" amesisitiza
Akasema viongozi watakaochaguliwa waweke mbali Ubwana na ufalme. Wawe watumishi wema wa waislamu na washaurike.
"Ile desturi ya kujipa nguvu ya maamuzi na mamlaka ya kusema na kufanya lolote haitusaidii. Kuna watu wanaifanya ndiyo njia ya kujiimarisha. Wanatisha watu. Ukiwa mtumishi mwema watu watakutii. Kwa nini uwatishe na kuwakandamiza? Jitathmini kwanza" ametoa rai.
Akawaomba waislamu watoe taarifa ya ukiukwaji wa haki (kwa dhamira njema) pasina kuongeza fitina na majungu.
"Nitapokea taarifa na kuzifanyia kazi. Majungu, fitina na chuki binafsi havitakuwa na nafasi. Lakini tutazifanyia kazi taarifa hizo kwa uadilifu mkubwa" amesema.
VIONGOZI WA KUTEULIWA
Kwa upande wa viongozi wa kuteuliwa katibu huyo mkuu amesema chekeche litafanya kazi. Amesema upembuzi yakinifu unaendelea na viongozi wasiofaa watawekwa pembeni
Alhaj mruma akasema bayana kwamba haridhishwi na utendaji wa baadhi ya makatibu wa mikoa na wilaya, akasema Mabadiliko yaliyofanywa hivi karibuni huko Katavi, Mwanza, Dodoma, Kaliua na Maswa yataendelea mikoa na wilaya zingine.
"Hatuwezi kuvumilia watu wanaotuchelewesha, wasiofanya kazi, wasioleta taarifa na ambao wanaficha taarifa za mapato na matumizi kwa makusudi"
Amesema na kuendea kufafanua "Kuna viongozi waliojimilikisha mikoa na hata wilaya. Hawafanyii kazi maelekezo ya ngazi za juu na maamuzi halali ya vikao. Ni wafalme na watawala wanaoendeleza ubinafsi. Hatutawavumilia"
........
Katibu mkuu wa BAKWATA ndiye mkurugenzi mkuu wa uchaguzi huo. Atakasimu madaraka kwa viongozi wa mikoa na wilaya ili wawe wasimamizi wa uchaguzi kwenye maeneo yao.
Waraka nambari moja ulioelekezwa kwa makatibu wa mikoa na wilaya utafuatiwa na waraka wa pili utakaoelekeza mengi ikiwa ni pamoja tarehe halisi na siku ya uchaguzi wa kila ngazi.
Nakala ya waraka nambari moja pia imefikishwa (kwa taarifa) kwa samaha Mufti, Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini, Mwenyekiti wa Halmashauri kuu, Masheikh wa mikoa na Wenyeviti wa mikoa
...........
