KUWAMA’S DAY 2015.
Umoja wa Kusaidiana Ukonga (KUWAMA) normally celebrates new year occasions in January. This year, the Executive Committee decided that the occasion be celebrated on the date close to 13.02.2015 when the Umoja attained 25 years of its existence- the Silver Jubilee. So the best date was 14.02.2015 which was also a Valentine Day. This was the first time the occasion was held at the organization’s own place, the Buyuni Gardens.
The Guest of Honour was Dr. Daniel K. Ndagala a PhD holder in Cultural Anthropology. Dr. Ndagala is a retired former Director of Cultural activity in the Government of United Republic of Tanzania.
There was a big sense of direction to the members in conceiving the idea of building a cultural house. His key note address has been reproduced to ensure that the powerful message is sent to all members and any interested person around the world.
Dr Ndagala addressed the members thus:-
“ NASAHA ZA DKT. DANIEL K. NDAGALA KWENYE SHEREHE YA UMOJA WA KUSAIDIANA UKONGA TAREHE 14 FEBRUARI 2015
Ndugu Mwenyekiti wa KUWAMA,
Ndugu Katibu wa KUWAMA,
Ndugu Wajumbe wa Kamati ya Uongozi,
Ndugu Wanachama wa KUWAMA,
Mabibi na Mabwana,
- Salaam Aleikum,
- Tumsifu Yesu Kristu
- Bwana Yesu Asifiwe
- Habari za Mchana.
Kwanza, namshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kuendelea kutupatia pumzi na afya njema hata tukaweza kuendelea na shughuli zetu mbalimbali leo hii. Pili, naushukuru uongozi wa Umoja wa Kusaidiana Ukonga kwa kunialika na kunipa fursa ya kushiriki tukio hili muhimu. Mwaliko huu umenifanya mmoja wa mashahidi wa mshikamano mlionao katika umoja wenu.
Asanteni sana.
Niruhusu niwadokeze kwamba umoja wenu ni tofali muhimu katika ujenzi wa jamii pana ya Watanzania. Kuta za nyumba imara hutokana na tofali moja moja imara zilizoshikamana. Kila mmoja wenu akiwa imara kutetea maslahi yenu na mkaendelea kushikamana ‘tofali’ hili litazidi kuwa imara na hivyo kusaidia katika ujenzi wa nyumba imara iitwayo Tanzania. Nawapongeza sana kwa kuanzisha umoja wenu huu miongo miwili na nusu iliyopita. Na kwa tathmini yangu ya haraka kuhusu niliyoyaona na kuelezwa, mbegu mliyoipanda tarehe 13 Februari 1990 imeota na kukua na mti unatoa maua kuashiria kupatikana kwa matunda muda si mrefu ujao. Tusiache kuumwagilia maji na kuupalilia mti wetu huu.
Ndugu Wana KUWAMA,
Nimefurahishwa na mipango yenu mizuri na nawatakia mafanikio. Ukitaka kufanikiwa ni
1
vema ukiwa na ndoto. Na ndoto nzuri ni zile za mchana, hasa ukiwa macho. Kuota ukiwa macho ni kule kuwaza vitu vikubwa na halafu ukatafuta njia halali za kuvipata vitu hivyo. Ninyi tayari mmeota na mmekwishaandaa namna ya kutimiza ndoto zenu hizo. Niwatie moyo; shirikianeni kutimiza ndoto zenu hizo. Naomba sasa nishirikiane nanyi katika kufikia ndoto zenu hizo kwa kutoa maoni kwenye maeneo mawili yafuatayo:
- Wawekezaji, na
- Utamaduni
Jambo la kwanza nimeona niligusie tu kwa ushauri maana mmelitaja katika risala yenu, na lina uhusiano na hili la pili ambalo mmeniomba nilizungumzie.
Wawekezaji
Huko nyuma, hasa katika miongo mitatu ya kwanza ya ujenzi wa taifa letu, tuliongozwa na siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Rais wa Kwanza wa taifa letu aliwahi kusema kuwa ili tuendelee tunahitaji vitu vinne: watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Kwa bahati mbaya,siku hizi hatuzungumziisana mambo haya manne wala kujitegemea. Badala ya kujitegemea tunahusudu sana kuwezeshwa. Na tumefika mahali pa kuamini kuwa wawezeshaji ni hao wanaoitwa wawekezaji. Tumeacha desturi nzuri ya jadi ya kujitegemea na kwenda kwenye desturi mbaya ya kusubiri kuwezeshwa. Zamani mtu alisema kwa kujiamini, “Usiniambie hivyo, sili kwako” au “Namshukuru sana Mungu maana sasa naishi kwangu”. Yote haya yalikuwa ni kuthibitisha kuwa mnenaji anajitegemea na kwa hiyo ni mtu huru. Kutokuthamini kujitegemea ni kujipiga ulemavu.
Mimi binafsi bado natambua kuwa ili tuendelee tunahitaji vitu vilevile vinne. Na hao wawekezaji wanatambua hivyo hivyo na ndiyo maana wote wanakimbilia kwanza ardhi kwa kuwa hawana. Wanafahamu kuwa fedha zipo au zitapatikana maana benki zipo na kazi kubwa ya benki zote ni kutoa fedha (kwa mikopo). Aidha wanatambua kwamba watu wapo (sisi Watanzania na amani yetu), siasa iliyopo haiwanyanyapai wawekezaji, na uongozi wa shughuli zao ni wao wenyewe. Kitu adimu kwa wawekezaji, hasa wageni, ni ardhi yenye ubora kama ya Tanzania.
Ndugu Mwenyekiti,
Ningependa niwaase wanachama wa KUWAMA kwamba katika kutekeleza mipango yenu msitumbukie kwenye kaulimbiu isemayo ‘Tukiwezeshwa tunaweza’. Kawaida mtu
2
anawezeshwa pale ambapo hawezi, lakini ninyi mnaweza. Ninyi ndiyo watu wenyewe,
mnayo ardhi na mnaendelea kutafuta ardhi. Endeleeni na uzi uleule maana watu tunaongezeka, lakini ardhi haiongezeki. Tafuteni ardhi nzuri na ya kutosha kabla haijamalizwa na hao wawekezaji. Ardhi ndiyo yenye madini, gesi, mafuta, misitu, rutuba ya kilimo, na kadhalika. Kwa wingi wenu, na siasa yenu ya kutaka kujiendeleza kiuchumu, na uongozi wenu madhubuti mnaweza kuendeleza maisha ya kila mwanachama wenu kwa kujitegemea. Mkiwa na vitu hivyo vinne mnakopesheka. Sisemi msitafute wawekezaji au ubia na wawekezaji, la hasha. Ninachosema ni kwamba tusiwe tegemezi kwa wageni ambao huenda wakachuma kwenye ardhi yenu na kuwaacha hoi huku ardhi yenu ikiwa ni mashimo au michanga mitupu. Kuweni makini katika kuandaa mikataba msije mkawa vihongwe au punda wa hao wawekezaji kwa ridhaa yenu wenyewe. Umoja wenu usiwe daraja la wageni kupata ardhi huku mkiwa wasindikizaji. Migogoro mingi ya ardhi baina ya Watanzania na wageni/ wawekezaji inatokana na maamuzi yaliyofanywa na Watanzania. Rai yangu ni kwamba kuweni makini. Pasipo ndicho, kisicho ndicho. Huwezi kupanda mwembe ukaota mpapai!
Utamaduni
Nimesikia nia yenu ya kujenga Jengo la Utamaduni ila nimeanza kujiuliza maswali mengi. Kwa mfano, je ni jengo la namna gani hili? Ni jengo litakalojengwa kwa njia na vifaa vya asili? Ni mahali pa kuchezea ngoma au ni kwa ajili ya matibabu ya jadi? Hivi mtu akiwauliza wana KUWAMA kuhusu utamaduni majibu yatafanana? Katika kutafuta majibu ya maswali haya nimeona kuwa ni vema nigeukiae kwanza dhana ya utamaduni ili tuelezane ‘utamaduni’ ni nini, ndipo tukubaliane ni utamaduni upi ambao wanachama wa KUWAMA wanataka kuujengea jengo. Kwa ruhusa yenu naomba nielezee kwa muhtasari mambo hayo ili mtakapojenga jengo hilo la utamaduni mpate kitu mlichokikusudia na ambacho kitaongeza thamani kwenye umoja wenu.
Utamaduni ni mchanganyiko wa taratibu za maarifa, imani, tabia, lugha, mawazo, mila, miiko, taasisi, nyenzo, stadi, kazi za sanaa, matambiko, sherehe, na vitu vingine vinavyohusiana na mambo hayo. Kwa maneno mengine, utamaduni ni changamoto la mambo mbalimbali yakiwemo ya kiroho, kimwili, kiakili na kihisia vinavyoitambulisha jamii au kikundi cha jamii. Unajumuisha siyo tu sanaa na fasihi, lakini pia mitindo ya maisha, haki za msingi za binadamu, na mifumo ya kuthamini vitu. Utamaduni huundwa na jamii. Kwa hiyo, tunapozungumzia utamaduni tunazungumzia mwenendo wa maisha wa jamii fulani. Kwa kuwa zipo jamii za aina mbalimbali zipo tamaduni za aina mbalimbali. Kuna tamaduni zitokanazo na kazi kuu za kujikimu kama vile uvuvi, kilimo, ufugaji n.k. Kila jamii ina utamaduni wake na tamaduni zinaweza kufanana kwa mambo fulani na zikatofautiana kwa mambo mengine. Tanzania ina jamii za kikabila zaidi ya 120, kila moja ikiwa na utamaduni wake. Tamaduni hizi zinafanana kwa mambo fulani na kutofautiana kwa mambo mengine. Hali hii siyo balaa bali ni vionjo vya utaifa wetu. Hivi ingekuwaje kama maua yote duniani yangekuwa meupe? Nimeelezwa kwamba wanachama wa KUWAMA mnatoka makabila mbalimbali, hivi kwenye Jengo lenu mtashughulika na utamaduni wa kabila lipi? Utamaduni siyo kama nguo ambayo utamwona mtu ameivaa na ukatambua kama ni shati au gauni. Utamaduni hujidhihirisha kupitia lugha, mila, desturi, imani, sanaa, burudani, malezi, uridhi n.k.
Ndugu Mwenyekiti na Wanachama,
Huenda hadi hapo baadhi ya wanachama wameanza kuhoji wazo la Jengo la Utamaduni. Lakini naomba niwatie moyo kwamba jengo hili ni muhimu sana. Tanzania ni nchi moja yenye jamii moja kubwa – taifa la Tanzania. Jamii hii haikuwepo miongo mitano na nusu iliyopita. Huko nyuma nchi ilikuwa ya makabila yanayohasimiana au kushirikiana kwa maslahi yao ya kikabila. Utaifa ulianza kujengwa wakati wa harakati za kutafuta uhuru, na juhudi za kujenga taifa lenye amani na mshikamano zikaendelea hadi sasa. Wakati wote huu zimekuwepo juhudi za kujenga na kuimarisha jamii ya kitaifa kwa kutumia jamii za kikabila kama nyenzo. Kumekuwepo juhudi za kujenga utamaduni wa taifa kwa kuyaendeleza yale yote mazuri ya tamaduni za makabila yetu na kuachana na yale yote mabaya ya tamaduni za makabila yetu. Kinachojitokeza ni jamii moja kubwa ya kitaifa inayoundwa na jamii nyingi ndogo ikiwemo hii ya kwenu Ukonga. Jamii hii inazo lugha nyingi za asili ambazo zinaendelea kuineemesha lugha yetu kuu Kiswahili. Utamaduni wetu wa taifa ni mzuri kwa kuwa umesheheni vionjo vingi sana vitokanavyo na tamaduni za jamii mbalimbali za nchi yetu. Vionjo hivi visipoendelezwa vitapotea milele. Sharti lugha zetu za asili, ngoma na sanaa zetu za jadi, hadithi na vitendawili, vyakula na mapishi ya asili, urembo wa asili, maadili, heshima na adabu vifundishwe na kuendelezwa ili kuneemesha utamaduni wa taifa letu. Mambo yote haya ni sawa na viungo vya chakula. Kila kiungo kinaweza kutumiwa peke yake, lakini vikiwekwa kwa pamoja kwenye mchuzi ndio starehe ya kitoweo. Tamaduni zote hizi ni zetu wote na zitakuwa zetu zaidi tukizielewa na kuzitumia kujenga mshikamano na umoja. Na hapa ndipo linapokuja suala la Jengo la Utamaduni.
Ndugu Mwenyekiti,
Nimesema hapo awali kwamba umoja wenu ni tofali imara la kujenga jamii yetu ya kitaifa. Kwa hiyo, jengo la utamaduni mnalolikusudia ingefaa liwe linalenga utamaduni mpana – utamaduni wa taifa. Liwe ni jengo ambamo:
- Mtajenga madaraja baina yenu wenyewe, na kati yenu na jamii nyingine. Hii ni kwa njia ya maonesho ya sanaa, filamu na michezo ya kuigiza.
- Mtaonyesha na kutangaza uanuwai wa utamaduni wetu kama vile mavazi ya sehemu mbalimbali za Tanzania mkianza na zile wanakotoka wanachama wenu.
- Mtawarithisha watoto wenu mambo mema ya jamii zetu na nchi yetu kwa njia ya hadithi, vitendawili na simulizi mbalimbali.
- Mtatunza na kukumbushana mambo ya zamani ya sehemu mbalimbali za nchi yetu kwa njia ya machapisho na maonyesho ya kimakumbusho.
- Mtaandaa shughuli mbalimbali za burudani kama vile ngoma, nyimbo, n.k.
- Mtabadilishana mapishi na vyakula vya jamii mbalimbali na kuwa kituo ambamo watakimbilia wale wanaotaka kuonja vyakula vya Tanzania.
- Mtawafunda watoto wenu wanapofikia hatua mbalimbali za makuzi pasipo kukiuka malengo ya taifa.
Ndugu Mwenyekiti,
Nimeongea kwa kirefu kuhusu dhana ya utamaduni kuonyesha umuhimu wa jengo la utamaduni katika kituo mnachokusudia kujenga. Nilitaka kutofautisha jengo la starehe na jengo la utamaduni. Jengo la utamaduni ni mahali pa kufahamiana na kushikamana. Kupitia programu mtakazoziandaa kwenye jengo hili tofauti zilizopo kati ya tamaduni za jamii mbalimbali zitakuwa mtaji wa kukuza na kutangaza utamaduni wa taifa letu na kuimarisha umoja wetu. Utamaduni wa taifa ni sawa na mti mkubwa wenye matawi mengi na mizizi mingi. Vyote vikiendelea kufanya kazi yake mti unadumu. Nimalize nasaha zangu kwa kuwatakia miongo mingine mingi ya mafanikio.
Asanteni kwa kunisikiliza”
Prior to that the Secretary of the Organization Cyriacus Boniface read the following key note address.
“RISALA KWA MGENI RASMI KWENYE SHEREHE YA KUAGA MWAKA 2014 NA KUKARIBISHA MWAKA 2015 SIKU YA KUWAMA (KUWAMA DAY) TAREHE 14.02.2015
Ndugu Mgeni Rasmi,
Tunayo furaha kubwa kukukaribisha kwenye sherehe yetu ambayo hufanyika kila mwaka. Leo ni mara yetu ya kwanza kufanyia sherehe hii katika sehemu tunayomiliki. Tunafurahi kuwa nawe kama mgeni rasmi katika eneo letu hili ambalo tunaendelea kuendeleza.
Umoja wetu umetimiza miaka 25 jana tarehe 13.02.2015 kwa kuwa ulianzishwa tarehe 13.2.1990 tulipopitisha Katiba yetu ya muda iliyotuongoza hadi tuliposajili rasmi Umoja wetu tarehe 28.01.2004 katika Wizara ya Mambo ya Ndani. Katika kipindi chote tumejenga Umoja, Mshikamano na Upendo kama nguzo na mtaji mkubwa. Mambo haya yalituingiza katika hatua ya kumiliki mali na hasa ardhi tuliposajili Wadhamini (Trustees) wetu tarehe 25.02.2009.
Ndugu Mgeni rasmi,tangu mwaka jana na hata mwaka huu Umoja wetu unandelea kuongozwa na Kauli Mbiu “KUWAMA na Maendeleo”. Lengo ni kuufanya Umoja uwe na uwezo wa kiuchumi wa kuweza kusukuma maendeleo ya wanachama wake na wana jamii kwa ujumla kwa kasi kubwa zaidi. Tunayo kamati ya miradi inayoishauri Kamati ya Utendaji kufanya kazi hii. Kamati yetu ya Utendaji ina wajumbe kutoka katika matawi saba wanaochaguliwa na Mkutano Mkuu kuhakikisha kuwa maamuzi yanafanyika kwa kuzingatia Demokrasia. Umoja una wanachama 150 na wanachama washiriki 120. Hivyo jumla tupo 270.
Mkutano Mkuu wa wanachama wote umekwisha amua kuwa eneo letu hili tunamofanyia sherehe lijengwe Jengo la Utamaduni . Sehemu nyingine ijengwe kumbi za starehe, hoteli, hostels, vyumba vya mikutano,vyumba vya kufanyia mihadhara(lecture rooms) maktaba, ofisi, apartments na maduka. Majengo yatachukua asilimia 33 (33%) ya eneo lote. Hadi saa mapendekezo ya ramani ya jengo la ghorofa nane yamekwisha pitishwa na wanachama na mazungumzo/mawasiliano na wawekezaji mbalimbali ikiwa ni pamoja na NHC, TIC na Warrenpark Worldwide Group yameanza na yanaendelea vizuri. Mkutano Mkuu pia umepitisha utafutaji wa ekari nyingine 50 karibu na Dar-es salaam kama mwendelezo wa shughuli za mahali hapa na hili nalo ni moja ya shughuli zinazoendelea.
Ndugu Mgeni rasmi, Mkutano Mkuu wa wanaumoja ulipitisha wazo la kuanzisha kijiji cha Umoja tukilenga kupata ekari 537 hapa Tanzania kwa ajili ya kilimo na huduma nyingine za Kijamii. Tumewaomba TIC pia kutusaidia kupata eneo hilo. Wakati huo huo, mmoja wa Wawekezaji tuliyemwendea ametutaka tuendelee kutafuta ardhi. Mwekezaji huyu ana mawazo mapana zaidi akionesha ana uwezo wa kujenga nyumba zinazofikia 10,000 katika vijiji mbalimbali hapa Tanzania kwa ajili ya makazi na kilimo. Wazo hili litaingia sasa katika hatua za kufanyiwa uchambuzi yakinifu hili lipate idhini ya Wanachama. Tunataka kuona ni namna gani litaingia katika mpango unaoendelea kubuniwa na Umoja wetu wa kujaza mapungufu (Filling Gaps) katika huduma za jamii. Tunalenga huduma tatu (1).Upunguzaji wa wana jamii wasiojua kusoma na kuandika( 2) Uboreshaji wa Elimu ya Sekondari na (3).Upunguzaji wa umaskini.
Tunataka kufanya hivyo kwa kutumia wanachama wetu waliostaafu au watakaostaafu au na wanajamii wengine wanaostaafu katika sehemu mbalimbali, kwa utaratibu maalum. Tunakusudia kuunda Timu Maalumu (Gap Filling Teams) kwa kazi hizi na katika maeneo yatakayoainishwa. Hivyo, wazo la Mwekezaji la kujenga nyumba za bei nafuu vijijini katika sehemu zenye maji ya asili,na kwa kutumia umeme wa jua na mkazo wa kutoharibu mazingira likifanyiwa utafiti wa kutosha, litatuwezesha kuzihusisha Halmashauri za Wilaya kama mbia wetu. Kituo cha Uwekezaji TIC kitahusika na tumeanza mazungumzo nao. Kupitia kwa Mwekezaji tuliyempata, Halmashauri zitalenga kuwajengea nyumba wafanyakazi wao vijijiji yaani walimu , waganga na maafisa wengine, lakini sisi tutalenga kupata ardhi na nyumba chache za Umoja/wanachama za kuufanya mpango wetu kuwa endelevu. Kwa hiyo suala zima la kutafuta ardhi ni moja ya agenda zinazoambatana na KUWAMA na Maendeleo.
Ndugu Mgeni rasmi, tunafahamu kwamba wewe umebobea katika fani ya Utamaduni. Nasi tumekupata katika hatua muafaka kwani tuko kwenye hatua ya kubuni hilo jengo la Utamaduni liweje na tuhusike na nini kama mchango wetu katika suala la Utamaduni hapa Tanzania. Ni kitu gani kitavutia watu wa aina mbalimbali kwa miaka mingi? Hakika tunahitaji mchango wako wa mawazo katika eneo hili na maeneo mengine tunayojaribu kusukuma katika hatua hii muhimu ya mipango.
Tunakushukuru. Tunakupenda. Tumefurahi kwamba umetambulika kwa wana Umoja kuwa mgeni rasmi wa kwanza kufika kwenye kiwanja chetu hiki ambacho tunaendelea kutafutia michango ya hali na mali ili kukiendeleza.
Karibu Sana. Mungu Akubariki.
UMOJA WA KUSAIDIANA UKONGA “