TANZANIA NA UZALENDO WETU TUMEKOSEA WAPI?
Uzalendo ni kitendo cha mtu kuipenda nchi yake, rasilimali zilizomo na watu wake kwa moyo wa dhati kwa kuilinda, kuithamini wakati wote na mahali popote.
Uzalendo katika nchi ndio chanzo cha maendeleo na usawa kwa watu wote nchini. Uzalendo unaleta haki, uzalendo unajenga misingi ya kujaliana, uzalendo ndio chachu ya matumizi ya rasilimali za nchi kwa usawa, uzalendo unatujengea undugu na amani, uzalendo unajenga na kudumisha upendo, uzalendo unajenga na kudumisha ushirikiano, uzalendo unajenga misingi ya uwajibikaji kwa wanajamii, uzalendo huondoa unyonyaji na matabaka katika jamii.
Uzalendo ni upendo na dhana ya hiari ya mtu binafsi uzalendo hujengwa kutoka moyoni mwa mtu, wakati mwingine uzalendo hujegwa na wanajamii kipitia misingi ya maisha wanayoyaishi na itikadi ya kisiasa miongoni mwa wanajamii. Hivyo mtu anaweza kuzaliwa akiwa mzalendo au itikadi ya kisiasa na misingi ya maisha katika jamii inaweza kumjenga mtu katika hali ya uzalendo.
Uzalendo unagawanywa katika aina mbili; a) uzalendo wa kihistoria ambao unatokana na maisha ya watu waliotangulia katika jamii. b) uzalendo wa kiutu. Huu ni uzalendo ambao huchukulia binadamu kama alivyo. Mfano katika Biblia maandiko yanasema mpende jirani yako kama nafsi yako.
Katika taifa letu dhana ya uzalendo imepotea miongoni mwa wanajamii. Historia inaonesha Tanzania imepitia vipindi mbalimbali; kipindi cha kabla ya ukoloni, wakati wa ukoloni, wakati wa kupigania uhuru na wakati baada ya uhuru. Kila kipindi kilijengwa na misingi yake ya uzalendo.
Kipindi kabla ya ukoloni historia inaonesha kuwa mababu zetu waliishi katika misingi ya umoja mshikamano na undugu, walifanya kazi kwa kushilikiana waliishi kama wamoja, rasilimali ziliwanufaisha wote watu wote walikuwa na haki sawa katika utumiaji wa rasilimali. Kipindi hiki kilitawaliwa sana na uzalendo wa kiutu.
Kipindi cha ukoloni. Historia inaonesha kuwa kipindi hiki wakoloni walitumia kila mbinu kuuvunja na kuundoa kabisa uzalendo miongoni mwa wanajamii. Walitujengea mioyo ya chuki, walituondolea umoja, walitujengea ubaguzi, walitugawa ili watutawale. Yote haya waliyafanya kwa manufaa yao binafsi ya kuzinyonya rasilimali za waafrika, walitumia Ardhi yetu kujinufaisha , walitumia udhaifu wetu kutufarakanisha, walitujengea matabaka katika jamii. walichonacho walikuwa nacho na wasiokuwa nacho waliendelea kukosa, elimu ilitolewa kwa misingi ya ubaguzi katika jamii, rasilimali za nchi zilitumika kuwanufaisha wachache wenye vyeo na madaraka tu. Hakika wakoloni walifanikiwa kutufarakanisha waafrika na kutuondolea uzalendo wetu.
Wakati wa kupigania uhuru. Hiki ni kipindi ambacho waafrika wenyewe tulianza kujijengea mioyo ya uzalendo tulioupoteza kupitia ukoloni, tulijijenga pamoja kushirikiana na kupambana dhidi ya ukoloni. Kipindi hiki mioyo ya uzalendo ilijegwa upya katika jamii ya watanzania. Baba wa Taifa alitumia juhudi zake kupitia Chama cha TANU kutuunganisha pamoja , tuwe wamoja , kutujengea upendo na baadae kushirikiana kudai uhuru wetu tukiwa kitu kimoja na wamoja.
Waasisi wetu walitumia juhudi zao kuujenga uzalendo na upendo katika jamii wakaiacha mizizi kwa mategemeo kwamba kizazi kilichofuata kingeendeleza hali ile.
Tanzania ya sasa si ile ya waasisi wetu, uzalendo tuliojengewa hatunao tena, umoja na mshikamano vimepotea sasa kila mtu akwenda kivyake nchi inapoteza mwelekeo , umasikini unakua kiuhalisia lakini unapungua kitakwimu, matabaka yanazidi kuongezeka makuadi wa kupoteza uzalendo wetu wanaongezeka kila siku, rasilimali sasa zinawanufaisha watu baadhi. Kwa mioyo migumu waliyo nayo sasa hata madaraka wanarithishana ili tu kujilinda. Taifa linahitaji jitihada za kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa tunautetea na kuuendeleza uzalendo wetu kwa maendeleo yetu . matabaka tuyaonayo leo ni matokeo ya kukosekana kwa uzalendo miongoni mwetu, misingi ya utu, ummoja, undugu sasa tumeipoteza kila mtu anafanya ajualo. Mabadiliko yanaletwa na mimi na wewe tumia nafasi yako vizuri kujenga usawa, utu, uwajibikaji, undugu katika jamii kwa maendeleo ya Taifa letu.