Quantcast
Channel: Envaya: Latest updates
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4212

Tanzania Social Support Foundation added a News update.

$
0
0

TANZANIA SOCIAL SUPPORT FOUNDATION
OFISI YA MKURUGENZI MKUU

TAARIFA KWA UMMA NA VYOMBO VYA HABARI


YAH: KUFUNGWA KWA MFUKO WA ELIMU YA JUU WA SHIRIKA LA TSSF


Hii ni kuutarifu umma wa wanachama wa Shirika la TSSF, wadau wa Shirika la TSSF, waombaji wote walioomba mikopo nafuu ya elimu kutoka Shirika la TSSF, vyombo vya habari, na umma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla kwamba, kwa kuzingatia utamaduni, misingi, na mila za utii wa raia kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwa kuzingatia kauli ya Serikali iliyotolewa mnamo tarehe 14 Novemba 2017 na Mhe. William Tate Ole Nasha ambaye ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo kauli hiyo ilisimamisha mara moja shughuli za utoaji mikopo zilizokuwa zinafanywa na Shirika la TSSF;
Kwa kuzingatia masharti ya kauli hiyo, ikiwa ni pamoja na kutii na kuiheshimu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Shirika la TSSF limesalimu amri kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kufunga rasmi Mfuko wa Elimu ya Juu wa Shirika la TSSF ambao ndio uliokuwa na wajibu wa kutoa mikopo nafuu ya elimu, ufadhili wa masomo ya elimu ya juu, gharama za matumizi wakati wa kuhudhuria masomo ya elimu ya juu, na punguzo la ada ya masomo ya elimu ya juu. Mfuko huo umefungwa rasmi kuanzia leo tarehe 18 Desemba 2017.
Sababu za kufungwa kwa Mfuko wa Elimu ya Juu wa Shirika la TSSF ni;
1. Amri ya Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya Jamhuri ya Muungano ambayo imetaka kusimamishwa kwa Shughuli za Utoaji Mikopo nafuu ya elimu ya Juu kutoka Shirika la TSSF.
2. Amri ya Msajili wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali ambaye amesimamisha shughuli zote za Shirika la TSSF ili kupisha uchunguzi unaofanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya tuhuma za utapeli zinazolikabili Shirika la TSSF.
3. Akaunti za Shirika la TSSF kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi ambapo Jeshi la Polisi limeomba amri ya Mahakama ili kuendelea kushikilia akaunti za Shirika la TSSF kwa miezi sita zaidi. Endapo kama Shauri hilo litasikilizwa na Jeshi la Polisi kuendelea kushikilia akaunti hizo, tafsiri yake ni kwamba akaunti hizo zitashikiliwa mpaka mwishoni mwa mwezi Juni 2018.
4. Kusimama na Kuchelewa kwa utekelezaji wa taratibu za kuhakiki fomu za maombi ambazo zilikuwa zimekusanywa, kuzipangia mikopo nafuu au aina nyingine ya ufadhili, pamoja na kuchakata miamala ya malipo ya mikopo nafuu kwa walengwa, pamoja na malipo ya ada kwa vyuo husika.
Ni dhahiri kwamba, muda umekwenda sana na kwamba kwa sasa wanafunzi wanakaribia kufanya mitihani wakati ambapo Shirika la TSSF halina uwezo wala nyenzo za kuwezesha lolote kutekelezeka kwa wakati kutokana na Serikali kuweka zuio na kushikilia nyenzo zote ambazo Shirika la TSSF lilikuwa likizitumia katika kufanya shughuli zake.

Kutokana na uamuzi huo wa kufunga shughuli za Mfuko wa Elimu ya Juu, na baada ya kufanya tafakuri ya kina, Shirika la TSSF limeona kuwa hakuna sababu ya kugombania fito au tofali wakati nyumba tunayoijenga ni moja. Kwa mantiki hiyo, Shirika la TSSF limeamua kufanya yafuatayo;
1. Kuungana na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa njia ya kuwezesha upatikanaji wa fedha zitakazowezesha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ya Jamhuri ya Muungano kuwahudumia Wanafunzi Wengi Zaidi


Shirika la TSSF linatangaza nia yake hadharani ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kugharamia mafunzo ya elimu ya juu kwa njia ya kuwezesha kupatikana kwa fedha ambazo zitatunisha mfuko wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu na hivyo kuifanya Bodi hiyo kuweza kuhudumia wanafunzi wengi zaidi. Uwezeshaji huo ni pamoja na kubuni programu mbalimbali ambazo zitawezesha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi na hivyo kuweza kufikia malengo ya kuhakikisha kuwa kila Mtanzania mwenye sifa za kupata elimu ya juu anapata elimu hiyo. Katika kufanikisha azma hiyo, Shirika la TSSF litafanya maandikiano na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kuweza kufanikisha mazungumzo, taratibu na masuala mengine ambayo yatawezesha kufanikiwa kwa azma hiyo chini ya Mpango wa Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi yaani (Public – Private Partnership).
Ni imani ya Shirika la TSSF kwamba, kwa kuwa Serikali yetu ni sikivu, inayojali wanyonge, na iliyojizatiti katika kukuza na kuwezesha ukuaji wa sekta binafsi hapa nchini, itatupokea kwa furaha na itatushauri, kutukosoa pamoja na kutuongoza vyema ili kuhakikisha kwamba, azma hiyo inafanikiwa, na inatekelezeka kwa ajili ya ustawi wa elimu ya juu hapa nchini. Ni imani yetu kwamba, kama mapokezi ya nia hii yatakuwa mazuri kama tunavyotarajia, matunda ya utekelezaji wa azma hii yataanza kuonekana kuanzia Mwaka ujao wa masomo wa 2018/2019.


2. Kurejesha Malipo Mbalimbali yaliyopokelewa na Shirika la TSSF kwa niaba ya ya Mfuko wake wa Elimu ya Juu


Kwa kuzingatia masharti ya kanuni za uanachama wa Shirika la TSSF, 2014 hasa Fungu la 18, 19, 20(b), 21(b), 23, 24(b), 27, na 28 zote yakisomwa kwa pamoja, yafuatayo yatafanyika;
2.1 Kwa kuwa wote ambao waliomba mikopo ya elimu ya juu kutoka TSSF ni wanachama halali wa Shirika la TSSF kutokana na kulipa ada ya fomu ya maombi kama inavyoelezwa kwenye Fungu la 19, 20(b), 21(b) na 23 la Kanuni za Uanachama wa Shirika la TSSF, toleo la Mwaka 2014 watastahili kurejeshewa malipo mbalimbali yaliyokusanywa kutoka kwao endapo kama wataamua kujiondoa kwenye Shirika la TSSF kama inavyofafanuliwa kwenye Fungu la 27 na la 28 la Kanuni za Uanachama za TSSF toleo la 2014. Wale watakaopenda kuwa wanachama wa TSSF kwa hiari yao wenyewe hawatazuiwa kufanya hivyo.
2.2 Fedha zote zilizolipwa kwa Shirika la TSSF kama ada mbalimbali za kuombea mikopo, zipo kwenye akaunti za Shirika la TSSF na zipo salama. Kwa kuwa akaunti hizo zinashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi, Uongozi wa Shirika la TSSF hauwezi kufanya muamala wowote iwe ni kuweka au kutoa. Kwa mantiki hiyo, TSSF haiwezi kufanya marejesho yoyote ya fedha kwa wanachama wake kwa sasa. Kwa kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na Uchunguzi wake dhidi ya tuhuma za Utapeli dhidi ya Shirika la TSSF, na kwa kuwa Maafisa wa Shirika la TSSF hawawezi kufanya shughuli yoyote kwa sasa kutokana na Ofisi za TSSF kufungiwa kwa muda na Msajili, na kwa kuwa TSSF inatambua kwamba wapo wanachama wake ambao walilipa ada za fomu lakini fomu zao hazikuwa zimefika TSSF kutokana na sintofahamu kadhaa zilizojitokeza hivi karibuni, utaratibu wa kurejesha malipo yote kwa wale watakaojiondoa TSSF utakuwa kama ifuatavyo;
2.2.1 Uongozi wa Shirika la TSSF utaharakisha jitihada zake za kuhakikisha kuwa Ofisi zake zinafunguliwa na huduma ka kiofisi na kiutawala ambazo siyo za utoaji wa mikopo zinarejea kama kawaida.
2.2.2 Baada ya huduma za kiofisi kurejea, na akaunti za Shirika la TSSF kufunguliwa, Shirika la TSSF litatoa fomu ya madai (Claim Form) ambayo itajazwa na wale wote ambao walilipa malipo mbalimbali kwa TSSF kisha TSSF itahakiki madai hayo na kuyalipa kwa wahusika.
2.2.3 Wale ambao watapenda kuendelea kuwa wanachama wa TSSF watajaza fomu za kuhuisha taarifa zao.
2.2.4 Kuhusu suala la ni lini malipo hayo yatakapoanza kulipwa, ni mpaka pale Jeshi la Polisi litakavyo achilia akaunti za TSSF. Taarifa kuhusu kufunguliwa kwa akaunti hizo, na kuanza mchakato wa madai na malipo zitatangazwa hapo baadae.
3. Kuhusu Barua zilizoandikwa vyuoni kama Dhamana kwa Waliokuwa Wamepangiwa Mikopo katika Awamu ya Kwanza
3.1 Barua Zilizowasilishwa Vyuoni kama Dhamana
Shirika la TSSF litaviandikia vyuo vyote ambavyo viliandikiwa barua za dhamana, kusitisha dhamana hizo kutokana na kufungwa kwa Mfuko wa Elimu ya Juu wa Shirika la TSSF. Wale wote ambao walikuwa wamepewa barua hizo za dhamana pamoja na wale wote waliokuwa wameomba mikopo nafuu ya elimu kutoka TSSF wanashauriwa kutafuta vyanzo vingine vya ufadhili ili waweze kugharamia masomo yao.
3.2 Waliokuwa Wamepangiwa Mikopo katika Awamu ya Kwanza
Hii ni kuwataarifu wale wote ambao walikuwa wamepangiwa mikopo nafuu ya elimu katika awamu ya kwanza kwamba, mikopo yao imefutwa kutokana na kufungwa kwa Mfuko wa Elimu ya Juu wa Shirika la TSSF. Wale wote ambao walipangiwa mikopo hiyo nao wanastahili kurejeshewa malipo yote ambayo walikuwa wamelipa kwa TSSF kama watajiondoa kwenye Shirika la TSSF na wanashauriwa kutafuata ufadhili wa masomo yao kutoka kwenye vyanzo vingine ili waweze kugharamia masomo yao.
4. Maendeleo ya Shirika la TSSF
Kwa kuzingatia misingi ya historia ya Shirika la TSSF tangu Mwaka 2011, Shirika la TSSF litaendelea na shughuli zake za kuboresha huduma za afya, uchumi hasa kwa vijana, utalii na utawala bora.

Imetolewa na:


Donati Primi Salla
MKURUGENZI MKUU
18 Desemba 2017


Viewing all articles
Browse latest Browse all 4212

Trending Articles