GULUKA KWALALA YOUTH ENVIRONMENT GROUP KWA SASA INATEKELEZA MRADI WA KUIMARISHA UTAWALA BORA KATIKA USIMAMIZI WA MALIASILI (NRM) KATIKA KATA ZA KURUI, MAFIZI, VIJINGO NA KISARAWE ZILIZOPO WILAYA YA KISARAWE NA KATA ZA BUPU SHUNGUBWENI NA MKAMBA ZILIZOPO WILAYA YA MKURANGA . MRADI HUU ULIANZA KUTEKELEZWA MWAKA 2009 NA UTAMALIZIKA MWAKA 2012.
MAFANIKIO YA MRADI WA KUIMARISHA UTAWALA BORA KATIKA USIMAMIZI WA RASILIMI ZA MALIASILI.
- Kila kata iliyoko ndani ya mradi huu ilianzishiwa kamati ya usimamizi wa rasilimali za maliasili (NRM). Kamati hiyo ilikuwa na wajumbe 15 ambao walitoka kila kijiji ndani ya kata husika.
- Tulifanikisha kuzisajili kamati hizo kuwa CBO. Kwa sasa tuna CBO's saba ambazo zinajishughulisha na usimamizi wa rasilimali za malisili katika kata za Kuruhi, Marui, Vihingo, Kisarawe, Shungubweni, Mkamba na Bupu ambazo zinashirikiana na serikali za vijiji.
- Tumejenga uhusiano mzuri baina ya serikali vijiji, halmashauri, Serikali kuu na Wananchi.
- Watu wameelewa kuhoji juu ya mapato na matumizi ya halmashauri ya kijiji kuhusiana na mirahaba wanayopewa na serikali kuu kutokana na uvunaji wa maliasili katika maeneo yao.
- Jamii inatoa taarifa kwa Serikali pale wanapoona kuna uhalibifu wa maliasili zinazowazunguka.
Kuna manufaa tuliyoyapata kutokana na mradi uliopita wa mwaka 2005 wa SERA YA TAIFA YA MAZINGIRA YA MWAKA 1997, SHERIA YA MAZINGIRA YA MWAKA 2004 NA MKAKATI WA TAIFA WA HIFADHI ARDHI ZA VYANZO VYA MAJI
Mradi wa sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 1997 umeleta mabadiliko makubwa katika kijiji cha Kisanga na Kata nzima. Kwanza wanajamii wa Kata ya Masaki wamepata Elimu juu ya Elimu ya Mazingira. Kwani kabla ya mradi huu kulikuwa hakuna Program mahususi ya uelimishaji umma kuhusu umuhimu wa hifadhi ya mazingira. Sasa vijiji vya Sungwi, Masaki, Gumba na Kisanga vyote vya Kata ya Masaki Wilaya ya Kisarawe vina Program juu ya hifadhi Mazingira kupitia kamati ya ardhi na mazingira ya vijiji. Hivyo hizo kamati zinajukumu la kuelezea umma juu ya matatizo makuu sita ya kimazingira.
1. Uharibifu wa ardhi
2. Kutokupatikana kwa maji safi kwa wakazi wa mijini na vijijini.
3. Uchafuzi wa mazingira
4. Upotevu wa viumbe na Makazi ya viumbe pori na BIOANUAI
5. Uharibifu wa makazi ya viumbe wa majini
6. Uharibifu wa misitu.
Hivyo jamii ya Kata ya Masaki baada ya kuelewa hayo matatizo. Kila kijiji ilyafanyia kazi.
Mfano: Kijiji cha Kisanga kilianza na tatizo na mbili (2) kutopatikana kwa maji safi kwa wakazi wa mijini na vijijini. Kabla ya kuanza kutekeleza huu mradi wathirika walikuwa wanawake waliamka usiku wa saa 10:00 kwenda kutafuta maji na wanatembea sio chini ya km 4 hadi km 5. Kwa siku, walikuwa wanarudi na ndoo moja muda wa saa 4:00 Asubuhi.
Hivyo kutokana na uhamasishaji wa Guluka Kwalala Youth Environment Group. Ilibidi Wanakijiji wa Kisanga kutekeleza sera ya taifa ya mazingira ya mwaka 1997 na sheria ya mazingira ya mwaka 2004. Watu wote waliokuwa ndani ya mita 60 ilibidi waamishwe ili kulinda vyanzo vya maji na zoezi hilo liliungwa mkono na Mheshimiwa Khanifa M. Karamagi wakati huo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe.
Baada ya zoezi hilo la utekelezaji wa sera ya Taifa ya mazinga ya mwaka 1997. Leo hii Kijiji cha Kisanga tatizo la maji linapungua na akina mama hawaamki usiku na kutembea umbali mrefu. Wanatembea umbali wa km 1. Na kupata maji safi na salama kwa wakati. Hivyo inawasaidia nao kushiriki katika uzalishaji mali na kuongeza kipato cha familia. Kwa sasa familia zimeanza kupunguza umaskini uliokithiri miongoni mwao.
Tatizo lingine tulilolishughulikia ni uharibifu wa ardhi. Kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi huu wa vijiji vya Wilaya ya Kisarawe hususani kijiji wa Kisanga walikuwa wanalima au kupalilia mikorosho kwa moto. Kwa kufanya hivi walikuwa wanapata mazao machache na kuona kilimo hakina maana na wanakijiji wakaanza kukata mazao. Mfano Miembe, Mikorosho kwa kutengeneza mkaa na kuacha kulima kilimo cha mihogo .
Baada ya kupata elimu ya mazingira na kuacha tabia ya kupalilia kwa kutumia moto, wanajamii wa kijiji cha Kisanga wameanzisha kilimo msitu na kuongeza pato la kujikimu na mazao ya korosho kwa sasa wanauza gharani. Hivyo kilimo kimeanza kuboresha maisha yao kwa kujenga nyumba za bati na kupeleka watoto shule. Hayo ndio mafanikio ya awali yaliyoanza kuonekana kwenye kijiji cha Kisanga.
Pili Wanakijiji cha Panga la Mwingereza Kata ya Vikumbulu Wilaya ya Kisarawe hiki kijiji kinapakana na pori la Taifa la Selous kulikuwa na uharibifu mkubwa wa upotevu wa viumbe na makazi ya viumbe pori na BIOANUAI na tatizo lingine ni uharibifu wa mazingira.
Baadhi ya Jamii inayozunguka pori la taifa la Selous. Iliona hili pori ni mali ya serikali kuu. Na haliwanufaishi chochote. Na hii ilichangiwa kutoshirikishwa serikali ya kijiji katika kuhakiki au utoaji vibari vya uwindaji. Lakini baada ya utekelezaji mradi huu. Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe imetekeleza Program ya mpango bora wa matumizi ya ardhi na inatoa mrahaba inayotokana na uwindaji kwa serikali ya kijiji.
Hivyo jamii ya Panga la Mwingereza (Kisarawe) kwa sasa inaona kuwa pori la Selou ni mali yao. Hivyo jamii inahifadhi makazi ya viumbe pori na BIOANUAI.
Vijana na akina Mama wameanzisha vikundi vya ufugaji nyuki. Kwa kufanya hivyo wanahifadhi misitu na kuwaongezea kipato.
Vikundi vya ufugaji nyuki. Vinavuna Asali mara mbili kwa mwaka. Na kuongeza kipato kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka kwa kupunguza umasikini, na Jamii ya Panga la Mwingereza wanalima milima kwa mtindo wa ngoro (matuta kukinga milima) kwa kufanya hivyo wameboresha hali ya mazingira kwa kuzuia mmomonyoko wa ardhi.
Hayo ni baadhi ya mafanikio machache tuliyopata kutokana na utekelezaji wa mradi wa SERA YA TAIFA YA MAZINGIRA YA MWAKA 1997, SHERIA YA MAZINGIRA YA MWAKA 2004 NA MKAKATI WA TAIFA WA HIFADHI ARDHI ZA VYANZO VYA MAJI